WAZIRI MKUU AZINDUA KAMATI YA KITAIFA AFCON 2027
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Julai 05, 2024 amezindua Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) na kuahidi kuwa Serikali itafanya nayo kazi kwa karibu ili iweze kufanikisha malengo ya Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo kwenye hafla iliyofanyika katika hotel ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ina imani kubwa na kamati hiyo kwamba itapata mafanikio.
“Tuambieni tufanye nini ili tuwe mabingwa, kusanyiko hili liibue nini tufanye sasa na tuanze leo kufanya maandalizi. Tumeunda kamati yenye weledi na wataalamu kwenye sekta ya michezo, tunategemea itupeleke kwenye mafanikio makubwa. Uwepo wenu ni imani ya Serikali kwamba mnaweza kusimamia suala hili.”
Amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya maandalizi ikiwemo maboresho ya miundombinu ya viwanja, barabara, reli, anga na usafiri wa maji. “Serikali tumejiweka vizuri kuwa mwenyeji wa mashindano haya; sifa, uwezo na dhamira ya kufanikisha mashindano haya tunayo,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mashindano hayo yataongeza idadi ya wageni na watalii hapa nchini, ambao watakuja kwa ajili ya kutazama mashindano na matukio yanayohusiana na AFCON 2027. “Hii itasaidia kuongeza mapato ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.”