Vijana Na Michezo

UNGUJA YATAMBA UMITASHUMTA SOKA WAVULANA

0:00

 

 

Timu ya mpira wa miguu ya wavulana kutoka Mkoa wa Unguja Visiwani Zanzibar, imeibuka na ushindi mnono baada ya kuifunga Songwe kwa jumla ya magoli 6-1 katika muendelezo wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) inayofanyika Mjini Tabora.

Mchezo huo wa kusisimua umechezwa leo Tarehe 7 Juni 2024 majira ya saa 9 Alasiri kwenye Uwanja A wa Shule ya Sekondari Tabora Wavulana, na kushuhudiwa Nahondha wa timu ya Unguja Ismail Juma Ngwadi akifunga magoli 5 peke yake.

Kocha wa timu ya Unguja Mali Mdau, amewapongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo huo ambao ameeleza kuwa ni ushindi muhimu waliokuwa wakiuhitaji ili kujiweka vizuri kwenye nafasi ya kuingia hatua ya robo fainali.

Kwa upande wake Nahodha wa timu ya Unguja Ismail Juma Ngwadi, amesema mchezo walioshinda dhidi ya songwe ni ishara njema kuwa pamoja na ugumu wa michezo ya mwaka huu lakini bado wanaweza kushindana na kupata matokeo.

Kocha wa Timu ya mkoa wa Songwe Halimoja Mohamed Ramboka, amesema wamepoteza mchezo wao kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini pamoja na kipigo hicho kutoka Unguja bado wanayo nafasi ya kujiuliza katika michezo mingine inayofuata.

Mchezo mwingine uliochezwa katika Uwanja wa B wa Shule ya Sekondari Tabora Wavulana, ulizikutanisha timu za Mikoa ya Arusha na Iringa, ambao hadi muda wake unamalizika Arusha ilikuwa na ushindi wa magoli 2-0.

Mashindano ya UMITASHUMTA & UMISETA 2024 yanayoendelea mkoani Tabora yananaandaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Juni 08,2024 na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim majaliwa kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Back to top button