Habari

NDEJEMBI AAGIZA HALMASHAURI KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI

0:00

NAIBU Wazir, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinakamilisha kwa wakati utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia mradi wa kuboresha shule za sekondari (SEQUIP) na mradi wa kuboresha shule za msingi (BOOST) ili kutumiwa  na wanafunzi watakaojiunga na shule hizo Januari, 2024.

Mhe Ndejembi ameyasema hayo kwenye ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alipokuwa akikagua ujenzi wa shule ya msingi Muungano na Mshikamano pamoja na Shule ya Sekondari tarajiwa ya Lwanjikolwa.

Akizungumza na viongozi na wataalamu wa Halmashauri hiyo, Mhe Ndejembi amepongeza kasi nzuri ya utekelezaji wa miradi huku akizitaka halmashauri nyingine kuiga mfano wa halmashauri hiyo katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

“Jitihada kubwa sana imefanywa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fedha hizi za maendeleo ambapo kazi yake inaonekana, sasa hatutegemei mtu yeyote arudishe nyuma jitihada hizi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuwahudumia wananchi wetu.”

“Miradi hii ya BOOST na SEQUIP tunatarajia yote ikamilike katika muda uliopangwa na ni maelekezo ya Serikali kwamba isiwepo halmashauri ambayo itashindwa kukamilisha ndani ya muda. Na siyo tu ikamilike bali thamani ya fedha iliyotumika ifanane na miradi. Hatutomchekea yeyote ambaye atashindwa kusimamia miradi hii kwa uadilifu,” amesema Mhe. Ndejembi.

Mhe Ndejembi pia amezitaka kamati zinazosimamia miradi hiyo kufanya kazi kwa umoja ili kuepuka migongano ambayo husababisha kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati lakini pia kushindwa kusimamia ufanisi wa kazi na kusababisha kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za umma.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Njeza ameishukuru serikali kwa kazi kubwa iliyofanya ya kupeleka miradi ya maendeleo ndani ya jimbo hilo huku akiahidi kushirikiana na wataalamu katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

” Jimbo letu hili tumeletewa miradi mingi ya maendeleo hii ya elimu katika shule za msingi na sekondari ikiwemo. Tunamshukuru sana Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na tunaahidi kwamba tutahakikisha tunaikamilisha kwa wakati ili azma yake ya kuwahudumia wananchi wa halmashauri ya wilaya ya mbeya iweze kutimia,” amesema Mbunge Njeza.

Back to top button