Habari

TUSHINDANE KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI-DKT.MWINYI

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wanasiasa kushindana kuwaletea wananchi huduma bora za kijamii kimaendeleo.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kama yeye amejenga hospitali kila Wilaya na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii iwe ni mashindano na siyo kuleta hoja za uvunjifu wa amani.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo wakati wa makabadhiano na ufunguzi nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Abdullah Mzee , Mkoa wa Kusini Pemba tarehe 01 Julai 2024.

Aidha Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza wananchi kuendelea kulinda , kudumisha amani na utulivu pamoja na kuiombea nchi katika uchaguzi mkuu mwakani.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kipindi cha mwaka mmoja kilichobaki hususani katika sekta ya afya, Serikali itatoa huduma bora za afya na kuboresha vituo vya afya vyote , ujenzi wa hospitali za Mikoa na kujenga hospitali kubwa ya rufaa ya  kimataifa ya Binguni.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa nyumba za Wafanyakazi wa sekta ya afya katika Wilaya za Unguja na Pemba.

Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar hususani katika sekta ya afya na kukamilisha mradi wa nyumba za Wafanyakazi katika Hospitali ya Abdullah Mzee wenye gharama za shilingi bilioni 16.5 za kitanzania

Back to top button