Habari

UWEKEZAJI KWENYE SEKTA YA ELIMU LAZIMA UMGUSE MWALIMU

0:00

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, uwekezaji wowote unaofanywa katika Sekta ya Elimu lazima umguse Mwalimu kwani ndiye injini na kiongozi wa rasilimali zote zinazowekwa kwenye mfumo wa elimu nchini.

Dkt. Biteko mesema hayo tarehe 13 Machi 2024 wakati alipomwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuzindua Programu ya Kuboresha Kada ya Ualimu nchini (GPETSP) katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam hafla ambayo ilienda pamoja na kaulimbiu ya Walimu Wetu Fahari yetu.

“Mwalimu ndiye rasilimali kuu inayofanya rasilimali nyingine ziweze kuleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Elimu, ndio maana mtaona programu tunayoizindua leo inaonesha kwa vitendo kuwa Serikali tunatambua kwamba lazima tuwekeze zaidi kwa Walimu  kwenye mazingira ya kujifunza na ufundishaji lakini pia kuwatambua Walimu kuwa ninyi ndio watu tunaowategemea kufanya elimu yetu iweze kwenda mbele.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila jitihada ili masuala yote yanayowahusu Walimu yafanyiwe kazi kwa kasi ikiwemo kuwapunguzia changamoto zinawazowakabili ili Walimu hao wajikite katika kusomesha na kutatua changamoto za watoto mashuleni.

Ameongeza kuwa,  kutokana na kazi nzuri ya Walimu hapa nchini, ufaulu wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi kwenda Sekondari umeongezeka kutoka 907,802  mwaka 2021 hadi 1,092,984  mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.4.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha bajeti ya Elimu ambapo katika mwaka 2021 fedha iliyotolewa ni shilingi Trilioni 4.7 na  kwa mwaka 2023 imeongezeka hadi shilingi Trilioni 5.7 sawa na asilimia 20.4.

Back to top button