Habari

NCHI WANACHAMA EAPP ZAKUBALIANA KUIPA MSUKUMO MIRADI YA UMEME

0:00

 

Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika  (EAPP Council of  Ministers-COM) limekubaliana  kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha.

Kukamilika  kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.(Transmission lines).

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko tarehe 27 Februari 2024 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za  Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of  Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi, Kenya.

“ Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada.” Amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa  kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP, hivyo inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na ndio maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ajili ya kujipatia nishati ya uhakika.

Amesema kuwa, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani.

Ameongeza kuwa, kuna upembuzi yakinifu unafanyika chini ya  Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tanzania hadi Uganda kutokea Shinyanga, ambao  utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera na pia kuwezesha nchi hizo kufanya biashara ya umeme.

Back to top button