MIL. 400 KUNUNUA VIFAA TIBA, MKINGA
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi amesema hadi kufikia Februari 2024 tayari kiasi cha Sh Milioni 400 zimepelekwa katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya Hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati ambapo taratibu za manunuzi zinaendelea.
Mhe Ndejembi ameyasema hayo wilayani hapo katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Philip Isdor Mpango.
“ Serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 ilileta kiasi cha Sh Milioni 300 za ununuzi wa vifaa tiba vinavyohitajika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika vituo vya afya na zahanati zilizokamilika.
Aidha vifaa hivyo vimenunuliwa na kufanikisha kuanza kutolewa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya na Zahanati 11 zilizokamilika. Hata hivyo hadi kufikia Februari mwaka huu kiasi cha Sh Milioni 400 zimeshaletwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya, Vituo na Zahanati,” Amesema Mhe Ndejembi.