WAFANYABIASHARA WADOGO, MAKUNDI MAALUM YAPEWE KIPAUMBELE UNUNUZI WA UMMA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania na wazingatie kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.
Amesema hayo tarehe 07 Februari, 2024 Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum katika masuala ya ununuzi wa umma.
“Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka makundi maalum. Na haya ni maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watanzania wote wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali na Binafsi wawezesheni watanzania kushika uchumi wa nchi na muone fahari katika hili.” Amesema Dkt. Biteko
Ameziagiza NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma na hatmaye kukuza Uchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, amesema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa, kusainiwa kwa hati hiyo kutaondoa mapungufu yaliyokuwa yakijitokeza kwenye masuala ya ununuzi wa umma hasa kwa watu wenye makundi maalum hivyo baada ya kusainiwa kwa hati hiyo utekelezaji wake utaanza mara moja