VYANZO VIPYA VYA UMEME KUANZISHWA KUKIDHI ONGEZEKO LA MAHITAJI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kutekeleza miradi mipya ya uzalishaji wa umeme badala ya kutegemea vyanzo vya zamani ili kuendana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 08 Februari, 2024 Jijini Dodoma baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Mkataba huo umesainiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kampuni ya Dongfang Electric International kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
“Lazima tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka, mahitaji ya umeme yameongezeka sana lakini vyanzo ni vilevile kwa miaka.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko vyanzo vyake, Serikali inaendelea kuongeza vyanzo vipya ikiwemo mradi wa Malagarasi ambao utekelezaji wake utachukua miezi 42 na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajia kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa mwezi huu.
Ameeleza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo mipya ni maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa vyanzo vyote vilivyopo vianze kujengwa sasa ukiwemo miradi ya umeme ya Kakono, Kikonge, Luhudji, Rumakali na miradi ya Gesi mkoani Mtwara ili kuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji ya nchi.
Aidha, ameishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 140 ili kutekeleza mradi wa Malagarasi ambapo Serikali ya Tanzania imetoa Dola za Marekani Milioni 4.14. Amesema Benki hiyo imeendelea kuiunga mkono Serikali katika miradi mbalimbali nchini.










