Habari

NAM IENDELEZE USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA ULINZI-MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wahakikishe wanashiriki katika kila tukio la umoja huo pamoja na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameyasema hayo jana Ijumaa, Januari 19, 2024 wakati akihutubia katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 – 20 Januari, 2024. Waziri Mkuu anamwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.

“Tumezungumzia hali ya mabadiliko ya tabia nchi na namna tunavyopata athari kwenye maeneo yetu na umuhimu wa kuweka mkakati wa namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye maeneo yetu.”

Masuala mengine ambayo Mheshimiwa Majaliwa aliyawekea msisitizo katika mkutano huo ni pamoja na kutoa wito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuangalia ajenda za NAM na kuona namna ya kushirikiana na NAM katika kuzitekeleza.

Mkutano huo wa siku mbili ulianza jana Ijumaa, Januari 19, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Speke Resort Kampala nchini Uganda. Katika mkutano huo Rais wa Uganda alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa kundi hilo.

Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti.

Mapema jana Januari 19, 2024, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Ranil Wickremesinghe ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana kuhusu kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili ikiwemo uwekezaji kwenye  sekta ya madini na biashara.

Naye, Sri Lanka Mheshimiwa Ranil Wickremesinghe alisema nchi yake ipo tayari kuwekeza nchini na amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wapo tayari kufungua ubalozi nchini Tanzania ili kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kurahisisha shughuli za uwekezaji na biashara.

Back to top button