Habari

Miradi ya BOOST yatekelezwa kwa asilimia 92, mikoa nane yashindwa kufikia lengo

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) umetekelezwa kwa asilimia 92.

Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa kikoa kazi na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo yake ya kusimamia ujenzi na kuona namna walivyojipanga katika kuwapokea wanafunzi wapya Januari, 2024.

“Katika maelekezo yangu nilielekeza kuwa miundombinu inayojengwa katika shule za masingi na sekondari ikamilishwe na isajiliwe kabla na ifikapo tarehe 31 Desemba mwaka 2023 ili kuwezesha kupokea wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanaotarajia kuanza masomo Januari 6 na8 mwaka 2024.”

Kati ya Aprili na Juni 2023 Serikali ilituma fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya na miundombinu ya elimu ya awali, msingi na sekondari katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mchengerwa amesema kati ya April na Juni mwaka huu, Serikali ilituma Sh bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 302 na ujenzi wa miundombinu kwenye shule za msingi zilizopo.

Amesema mpaka jana shule mpya za msingi 277 kati ya 302 sawa na asilimia 92 zimekamilika na shule 25 zipo hatua mbalimbali za ujenzi.

Ameitaja mikoa nane ambayo haijakamilisha ujenzi wa shule mpya hadi sasa kuwa ni Rukwa (Shule 07), Ruvuma (Shule 07), Dar es Salaam (Shule 04), Kigoma (03), Arusha (01), Manyara (01), Pwani (01) na Kilimanjaro (01).

Back to top button