Waziri Mchengerwa atoa maelekezo kwa TARURA

MTENDAJI Mkuu wa Wakala za Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ametakiwa kuwasisitiza mameneja wa TARURA ngazi ya mikoa na wilaya kutoa taarifa kwa wakurugenzi wa maeneo husika kuhusu makandarasi waliopo ili halmashauri ziweze kuwadai kodi ya huduma.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 23, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa katika kikao cha watumishi wa wakala huo.
“Mtendaji Mkuu sisitiza Mameneja wa TARURA ngazi za mikoa na wilaya ili watoe taarifa kwa wakurugenzi wa maeneo husika kuhusu Makandarasi waliopo ili halmashauri ziweze kuwadai Kodi ya Huduma.
“Ni vyema ukaangalia utaratibu wa uthibithisho wa malipo ya Kodi ya Huduma kabla ya kumlipa malipo yanayofuata,”amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema, TARURA inasimamia eneo kubwa la nchi ambalo linajumuisha wilaya 139 na halmashauri 184.
Waziri ameagiza, wakala huo kupitia wigo wa kiwango cha mikataba inayopaswa kutekelezwa ngazi ya wilaya kwani kwa sasa ni shilingi bilioni 3.
“Aidha, mameneja wa mikoa na wilaya wahusishwe katika usimamizi wa kazi zinazotekelezwa katika maeneo yao hata kama mkataba umesainiwa na makao makuu, wawe na uelewa na kazi zinazotekelezwa.
“TARURA kila mara ikumbuke kuwa inatekeleza majukumu yake chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI na si vinginevyo,”amebainisha Waziri huyo.
Vile vile, Waziri Mchengerwa amesema, TARURA ina jukumu la kusimamia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 144,429.77.
Pia amefafanua kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza fedha za matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara na madaraja.
“Ni kutoka Shilingi 275.03 mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi bilioni 836.237 kwa mwaka wa fedha wa 2021/22, 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 204 na mwaka huu wa 2023/24 bajeti ya TARURA imeongezwa zaidi hivyo kuwa katika wakati mzuri wa kutekeleza majukumu vizuri zaidi,”amefafanua Waziri Mchengerwa.










