DKT.MAHERA ATAKA USHIRIKIANO UIMARISHAJI HUDUMA ZA AFYA
Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Wilson Mahera Charles amewataka Waganga Wakuu wa Wilaya kutoa ushirikiano kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhusu taarifa za magonjwa ya mlipuko na udhibiti wake.
Dkt. Mahera ametoa maelekezo hayo jijini Arusha kwenye kikao maalum cha Kamati za Usimamizi wa Huduma za Afya za (CHMT) za Wilaya zote za Mkoa wa Arusha na Kamati ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa (RHMT) ambacho kimeshirikisha Wakurugenzi wa Halmashauri husika.
Kikao hicho kilichoendeshwa na Dkt. Mahera kililenga kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha huduma za afya, ustawi wa jamii na lishe ikiwemo udhibiti wa magojwa ya mlipuko kama surua, kuhara na kutapika.
“Ukweli ni kwamba ‘under coverage’ ni kubwa sana na ‘targeted group’ haijabainishwa lakini wametueleza mbinu za kubaisha tumieni shule watoto wanapatikana huko tunataka haya magonjwa yasitokee na mkirudi Wakurugenzi kaeni na watu wenu mjiongeze mfanye kila kinachowezekana muweze kuchanja ili kuzuia haya mambo yasiendelee,” amesema
Aidha amewataka waganga wakuu kupeleka taarifa kwa maandishi kwa wakurugenzi kuhusu fedha za mapato ya ndani zinapotengwa na kupelekwa kwenye Baraza la madiwani zipate idhini ya kubadilishiwa matumizi ili kukamilisha miradi ya afya na wananchi waanze kupatiwa huduma.
“Mkurugenzi akiamua madiwani hawawezi wakazuia fedha za mapato ya ndani sasa ikishindikana baadaye vituo havijaanza kufanyakazi tunasema DMO amezembea tunakula kichwa cha DMO kumbe hakupewa ushirikiano mzuri,” amesema.