WAWINDAJI WA KIENYEJI KUWEKEWA UTARATIBU MZURI” – WAZIRI MCHENGERWA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ( Mb), amesema Wizara inaandaa utaratibu mzuri kwa ajili ya kuongoza shughuli za uwindaji wa kienyeji.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo, leo Agosti 4, 2023 alipotembelea banda la TAWA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Nanenane), Mkoani Morogoro.
Waziri Mchengerwa amesema utaratibu huo utawekwa kwa ajili ya watanzania wanaopenda kufanya shughuli za uwindaji na utaendelea kusimamiwa na TAWA.
Sambamba na hilo, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuendelea kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha mchango wa utalii katika pato la Taifa unaongezeka.
“Mchango wetu katika pato la Taifa unakaribia shilingi Trillion Saba, tunataka tutoke Trillion Saba hadi Trillioni kumi, tukifanya kazi kwa bidii inawezekana” amesema Waziri Mchengerwa.
TAWA inashiriki katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kutangaza shughuli zake sambamba na fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo ufugaji wa wanyamapori.