Habari Tofauti

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo afurahia na jitihada zilizofanywa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amefurahishwa na jitihada zilizofanywa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) za kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili Ndani na Nje ya Nchi wa miaka 10 kuanzia 2022 hadi 2032.

Mkakati huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2022 umelenga kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa bidhaa itakayosaidia kutatua changamoto ya ajira kwa wasomi wa Kiswahili walio ndani ya nchi.

Waziri  Chana ameliagiza BAKITA kuwa na programu maalumu itakayowezesha kupatikana kwa mahitaji yanayotakiwa katika kutekeleza mkakati huo.

Aidha  ameagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinashiriki katika utekelezaji wa mkakati huo kwani ni mkakati wa taifa na kila Mtanzania anapaswa kushiriki katika kuutekeleza.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chana ameliagiza BAKITA kuhakikisha kila halmashauri nchini inapata nakalamango na nakalatepe ya Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili.

Amesisitiza kuhakikisha kuwa mkakati huo unatekelezwa kwa asilimia 100 kwa sababu utakuwa chachu ya ongezeko la pato la taifa kwa kuwa lugha ya Kiswahili inatumika kuvuta watalii nchini na kuongeza  kuwa kwa sasa soko la ukalimani limezidi kukua na kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika  wanahitaji Wakalimani. ” Serikali itahakikisha inawasilisha majina ya wataalamu wa ukalimani ili kukidhi haja ya ajira kwa wakalimani kwa sasa”, amebainisha Balozi Dkt. Chana

Akiwasilisha mkakati huo mbele ya  Balozi Dkt. Pindi Chana, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi, amesema kuwa dira ya Mkakati wa Taifa wa Ubidhaishaji wa Kiswahili ni kuwa na mfumo madhubuti wa kitaasisi katika kuratibu, kusimamia na kukuza maendeleo ya Kiswahili kitaifa, kikanda na kimataifa na dhima ya mkakati huo ni kusimamia, kuratibu na kushiriki kikamilifu katika kustawisha maendeleo na matumizi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

Bi. Consolata Mushi ameyasema hayo katika kikao maalumu kilichoketi baina ya Waziri Balozi Dkt. Chana na Menejimenti ya BAKITA kilicholenga kupitia mkakati huo ili kubaini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake.

Bi. Mushi ameeleza kuwa, mkakati huo umebainisha fursa mbalimbali za lugha ya Kiswahili ikiwamo kuuza machapisho mbalimbali ya Kiswahili ili kuinua vipaji na hali ya waandishi wazawa na kuongeza  kuwa lengo kuu la mkakati ni kukuza Kiswahili ili kiwe chachu ya maendeleo ya taifa.

Amebainisha kuwa BAKITA limeandaa kanzidata ya wataalamu mbalimbali wakiwamo wakalimani, wamilisi na wataalamu wa Kiswahili ambayo inakidhi mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa itakayosaidia kukidhi mahitaji ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi ambapo ili kukidhi haja hiyo, BAKITA linaendesha madarasa ya wakalimani ambapo hadi sasa linatambua wakalimani zaidi ya 90, pia linatoa Mafunzo ya Kuimarisha Stadi za Kufundisha Kiswahili kwa Wageni ambapo hadi sasa linatambua wataalamu 1,673.

Aidha, BAKITA linaendesha warsha kwa Wandishi wa Habari na Washereheshaji ili waweze kutumia Kiswahili fasaha.

Bi. Mushi amebainisha kuwa, kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, kuwa balozi zote za Tanzania zifungue vituo vya kufundishia Kiswahili na vituo hivyo vitumike kutangaza diplomasia ya uchumi, BAKITA limefanikiwa kufungua vituo katika nchi  10 ambazo ni Abu Dhabi, Italia, Nigeria, Uholanzi, Zimbabwe, Burundi, Ufaransa, Korea Kusini, Mauritius na Havana.

Ameongeza kuwa BAKITA linashirikiana na Idhaa za Kiswahili zaidi ya 300 duniani kote na kwamba  limekuwa likifanya mkutano wa Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili duniani kote mwezi Machi kila mwaka na ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya Kongamano la Idhaa za Kiswahili litakalofanyika Machi 2024.

Fauka ya hayo, Bi. Consolata Mushi ameeleza kuwa, ili kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Ubidhaishaji wa Kiswahili, BAKITA limeandaa mikakati kadhaa ya utekelezaji ikiwemo kuandaa vitabu na miongozo ya kufundishia na kujifunzia Kiswahili kwa wageni.

Ameeleza kuwa ili kukabiliana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, BAKITA linaandaa Kongoo ya Kiswahili ya Taifa ambayo itamwezesha mtumiaji wa lugha kutumia lugha ya Kiswahili fasaha mtandaoni.

Back to top button