MAJALIWA: DIASPORA TUNZENI HESHIMA YA TANZANIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanadiaspora wa Tanzania wazingatie sheria za nchi wanazoishi ili waendelee kutunza heshima ya nchi yao.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na Watanzania waishio St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.
“Baadhi yenu mko hapa mnatafuta fursa, na wengine wengi wako hapa kwa masomo. Zingatieni sheria za nchi hii, tunzeni heshima ya Tanzania. Teteeni Taifa la Tanzania, zungumzieni fursa zilizopo nyumbani,” alisema Waziri Mkuu.
Akisisitiza umuhimu wa kukitangaza Kiswahili, Waziri Mkuu alisema: “Kiswahili kiendelee kutangazwa kwa bidii kwani Kiswahili ni fursa na Kiswahili ni ajira. Tukitangaze Kiswahili na tushike nafasi za kutangaza lugha yetu kwa kasi kwa sababu tuna historia ya muda mrefu na Urusi ambao wamekuwa wakitumia lugha hii,” alisema.
Alisema katika baadhi ya vikao vyake na wawekezaji wa Kirusi, hakupata shida ya mkalimani kwa sababu walikuwa na mtu wao ambaye anatafsiri moja kwa moja kutoka Kirusi kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kirusi. “Lakini na sisi ubalozini kwetu tuna Afisa Uchumi ambaye alitusaidia kutafsiri Kiswahili kwenda Kirusi kwenye baadhi ya vikao. Tena aliongea kwa ufasaha zaidi. Tusiache fursa hii itupite,” aliwasisitiza.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapa picha halisi ya maendeleo na kiuchumi yanayofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, maji na akawahakikishia kwamba Tanzania iko salama, wao waweke bidii kwenye masomo yao.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk alisema mbali na kazi ya kudumisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya Diaspora.