RAIS DK.MWINYI AZIHIMIZA TAASISI KUWASILISHA MICHANGO ZSSF

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amezitaka Taasisi za Serikali na jumuiya zote za waajiri na waajiriwa wahakikishe wanawasilisha michango katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa wakati ili kurahisisha shughuli za uendeshaji wa mfuko huo katika kuwajengea misingi mizuri wafanyakazi wao wanapostaafu na kuhitaji mafao yao.
Ameyasema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na kuzindua mradi wa Mji wa Dk.Hussein Ali Mwinyi uliopo Mombasa Zanzibar pamoja na Mfumo wa huduma kwa wateja wa kuwasiliana wa ZSSF WhatsApp ukumbi wa Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha , Rais Dk.Mwinyi amewashauri wajasiriamali wote wajisajili na kuchangia Mfuko wa Hiari kupitia mfuko huo kwani una faida kubwa kwa biashara zao .
Vilevile, amewapongeza ZSSF kwa kuanza kulipa mafao mapya mawili kwa wanachama wake waliopoteza ajira na walioumia wakiwa kazini.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewapongeza ZSSF kwa kuzingatia utekelezaji wa agizo lake alilolitoa siku ya Wafanyakazi mei mosi mwaka 2023 kuongezeka kwa malipo ya pensheni kwa wastaafu.