WAZIRI MKUU ANENA: UWEKEZAJI UNA FAIDA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uwekezaji una faida na kwamba suala hilo siyo kitu kipya.
“Uwekezaji una faida, hata hapa mbele yetu (jirani na eneo la mkutano) kuna eneo la bandari limekodishwa na mtu ameweka uzio. Hawa watu wanakodisha maeneo na wanayalipia,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Ijumaa, Julai 07, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Bandari, mjini Mtwara.
Amesema mwekezaji wa kwanza kwenye bandari ya Dar es Salaam ambako uwekezaji unapigiwa kelele, mkataba wake ulikuwa na vipengele vyenye mapungufu, vikaboreshwa mwaka 2017 na akaongezewa miaka mitano.
Akifafanua kuhusu makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World, Waziri Mkuu amesema: “Ili mradi mmesema mkataba uzingatie maslahi ya Taifa, tutahakikisha mkataba huo unazingatia maslahi ya Taifa. Mmekuwa na hofu na ajira, hakuna atakayepoteza ajira. Mmekuwa na hofu na ardhi, kwamba anayekuja atachukua ardhi, siyo kweli. Hakuna mwekezaji aliyepewa ardhi kwa sababu hata kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha kukaa juu ya ardhi, na analipa kodi.”
“Hofu nyingine ni muda wa mkataba, mmesema atakaa miaka 100. Hapana, haijatamkwa popote ila akija tutakubaliana miaka ya kukaa na kufanya tathmini kadri tunavyoona ukaaji huo utakuwa na maslahi ya Watanzania.”
Amesema kampuni ya DP World imewekeza kwenye nchi nyingi duniani na imejenga bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. “Mwekezaji huyu anahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ana meli zaidi ya 400. Meli hizi zitaleta mizigo kwenye bandari yetu. Ninawaomba Watanzania tumwamini Rais wetu, ana nia njema sana ya kiuchumi ya kufungua milango.”