Habari Tofauti

UJENZI WA SHULE MPYA 302 ZA MSINGI KUONDOA MSONGAMANO WA WANAFUNZI

0:00

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema kupitia mradi wa BOOST, Serikali inaendelea na Ujenzi wa Shule mpya za Msingi 302 katika halmashauri zote nchini ili kuondoa msongamano kwenye shule zenye wanafunzi wengi zaidi ya 15,000.

 

Dkt. Msonde amesema hayo leo wakati akizungumza na  wananchi wilayani Mkuranga na Bagamoyo akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa shule hizo mpya.

Dkt. Msonde amesema Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza  shule za msingi zenye wanafunzi zaidi 1,500 kutafuta maeneo mengine ya kujenga ili  kuboresha utoaji wa elimu kwenye shule hizo.

Ameongeza kuwa, ili kutekeleza  maelekezo hayo, mnamo aprili 2023 Mhe. Rais aliiwezesha Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupeleka kiasi cha Shilingi Bilioni 230.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dkt. Msonde amefafanua kuwa, shule  hizo zitakuwa na jumla ya madarasa ya awali 604, madarasa ya msingi 3,276, majengo ya utawala 302 pamoja na matundu ya vyoo 6,160.

Dkt. Msonde amesema, ujenzi wa shule hizo unaenda sambamba na ujenzi wa madarasa 12,000 ya kisasa ya mfano kwa ajili ya wanafunzi wa awali nchi nzima.

Aidha, Dkt. Msonde amewahakikishia walimu kuwa, Serikali inaendelea  kutatua kero na malalamiko yanayohusu stahili na maslahi yao.

Dkt. Msonde akiwa katika ziara yake katika mkoa Pwani amekagua na kujionea ujenzi wa Shule mpya za Juhudi na Chatembo katika halmashauri ya Mkuranga pamoja na vyumba vya madarasa vya awali na msingi katika shule za Mtambani na Jitegemee katika wilaya ya Bagamoyo.

Back to top button