Waziri Mkuu akagua maendeleo ya ujenzi wa mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma

Leo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kuwa ifikapo Oktoba mwaka huu, majengo hayo yawe yamekamilika na kuwekwa samani, ili adhma ya Serikali ya watumishi kuhamia kwenye majengo hayo ifikapo Januari Mosi, 2024 itimie
“Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutaka kuona watumishi wote waliohamia Dodoma wanafanya kazi kwenye majengo rasmi fedha imetengwa, imetolewa na itaendelea kutolewa”
“Tafuteni mbinu za kiufundi za kukamilisha majengo haya kwa wakati bila kuathiri viwango”Moja ya mbinu ni kusimamia ujenzi huu usiku na mchana, tunataka tumalize majengo haya, Watanzania wanataka kuona majengo yanakamilika na kutumika.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wasimamizi wa ujenzi wa majengo kwenye mji wa Serikali watumie bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini
“Rais Dkt. Samia amesisitiza kuhusu uwekezaji na amekuwa akialika wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya bidhaa mbalimbali hapa nchini ikiwemo marumaru (tiles). Tutumie bidhaa zao badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.”