TANGA, MORO MABINGWA GOALBALL UMISSETA 2023
Mikoa ya Tanga na Morogoro imeibuka mabingwa wa mchezo wa Goal Ball wasichana na wavulana, ambao ni maalum kwa watu wenye uono hafifu ukiwa ni moja ya michezo iliyojumuishwa kwenye Mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA 2023) Mkoani Tabora.
Katika michezo ya fainali iliyochezwa Tarehe 22 Juni 2023 kwenye Ukumbi wa Chuo cha Uhazili Tabora, Timu ya mkoa wa Tanga Wasichana, iliifunga Singida 17-12 huku Rehema Ngwatu wa Tanga akiibuka mfungaji bora kwa kufunga magoli 16 peke yake.
Kwa upande wa Wavulana, Timu ya Goal ball ya Mkoa wa Morogoro imeibuka bingwa baada ya kuifunga Kilimanjaro 5-1 katika mchezo mwingine wa fainali uliochezwa Saa 5 Asubuhi.
Mchezo wa kutafuta nafasi ya tatu uliikutanisha Mikoa ya Ruvuma na Dodoma, ukahitimishwa kwa Dodoma kupata ushindi wa 11-9.
Michezo hii ya fainali imehitimisha michezo ya Goalball (Mpira wa goli) katika UMISSETA 2023 ambayo imeandaliwa kitaifa Mkoani Tabora.