WADAU WA MAZINGIRA WAKUTANA KUJADILI MAONI NA KUTHIBITISHA MABORESHO KATIKA KANUNI ZA UDHIBITI NA USIMAMIZI WA BIASHARA YA KABONI
Viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wadau wa Mazingira kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma na Binafsi, mashirika ya Kiraia na Wadau wa Maendeleo wamekutana kupitia maoni na kuthibitisha mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni.
Kanuni hizo zilipitishwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali No. 636 na 637 za tarehe 28 Oktoba mwaka 2022 zimekuwa kivutio cha uwekezaji katika eneo la upunguzaji wa ongezeko la gesijoto ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kikao hicho cha Wadau kimefanyika 21/6/2023 mkoani Dodoma na kufunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais( Mazingira), Dkt. Switbert Mkama.
Akiwaasilisha mada juu ya maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali, Bi. Risper Paul Koyi – Afisa Sheria Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa masuala ya Kaboni, amewashukuru wadau na kueleza kwamba maoni yote ya wadau yamezingatiwa katika mapendekezo ya maboresho ya Kanuni hizo.
Aidha, Bi. Risper aliwahakikishia washiriki wa kikao hicho kuwa, maoni yaliyopatikana kutokana na kikao yatazingatiwa katika kufanya maboresho katika Kanuni hizo na hatimae uweze kufaa Kwa matumizi na kuwa kivutio cha uwekezaji katika eneo la kupunguza ongezeko la gesijoto na kuiwezesha Tanzania kufikia lengo la kuchangia kupunguza ongezeko la gesijoto kwa asilimia 30-35 kufikia 2030.