Habari

WAZIRI MKUU:SERIKALI IMESAJILI MIRADI YA UWEKEZAJI 537

Ahmed Hassan

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali ilisajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,222.

Amesema hayo leo Alhamisi (Aprili 20, 2023) alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, kinachojengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center kwenye eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kuvutia wawekezaji kwa kupunguza kero na kurahisisha utoaji huduma.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa ongezeko la usajili wa miradi hiyo unatarajia kutoa  ajira takriban 92,770 “Kiwango hiki ni kikubwa kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961”

Amesema kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA)  imefanikiwa kusajili Miradi 38 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 139.70 na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 191.04.

“Miradi hiyo ni mahsusi katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na Kilimo, bidhaa za viwandani, bidhaa za Mifugo, bidhaa za Kemikali, bidhaa za madini na bidhaa za misitu”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kwani ni sehemu sahihi ya uwekezaji, na  kuleta mitaji yao “tunayo mazingira mazuri ya uwekezaji”

Akizungumzia kuhusu Mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kituo hicho kitakuwa na maduka zaidi ya elfu mbili, ambayo yatakuwa na ukubwa tofauti tofauti hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya wafanyabishara wa aina tofauti tofauti “Kutokana na ukweli huo, mtakubaliana nami kuwa kituo hiki kitapanua fursa ya Watanzania wengi kufanyabiashara katika eneo hili”

Back to top button