WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imeonesha Tanzania imepiga hatua katika kuwaletea maendeleo wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Maji, Elimu, Afya, na Mawasiliano.
Amesema hayo leo Jumamosi (Aprili 15, 2023) wakati alipozindua Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)-Tunguu. Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Seleman Abdulah.
Amesema kuwa katika Sekta ya Elimu, takwimu za Sensa zinaonesha kuwa kiwango cha jumla cha uandikishaji kwa wanafunzi ngazi ya shule za msingi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimefikia asilimia 95.9 Mwaka 2022 kutoka asilimia 94.6 ilivyokuwa Mwaka 2012.
“Kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wenye umri wa miaka 5 na kuendelea kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeongezeka hadi asilimia 79.1 mwaka 2022 kutoka asilimia 72.0 ilivyokuwa mwaka 2012”.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta ya maji matokeo ya Sensa yanaonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya vizuri kwa kuwa asilimia 99.5 ya kaya zote zina vyanzo vya maji ambapo kati ya vyanzo hivyo asilimia 67.8 ni vyanzo vilivyoboreshwa na asilimia 32.2 ni vyanzo ambavyo havijaboreshwa.
Kwa upande wa mawasiliano, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 97.5 ya Vitongoji/Mitaa/Shehia vimefikiwa na mitandao ya simu. “Kiwango hiki kinafanana na hali ilivyo kwa Tanzania Bara. Wakati huohuo Tanzania Zanzibar imefanya vizuri zaidi kwa kufikia asilimia 99.0 ya shehia ambazo zimefikiwa na mitandao ya simu”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote wapo kwenye umri wa miaka 15 hadi 64.
“Hii ni ishara nzuri katika maendeleo ya nchi, kidemographia umri huu unajulikana kama umri wa kufanya kazi Kwa maneno mengine, nchi yetu ina hazina kubwa ya nguvu kazi ambayo ni moja ya kichocheo katika kujenga uchumi imara”