Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Norway katika masuala ya maendeleo na hususan ufadhili wa miradi ya uhifadhi wa mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa leo Machi 21, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba wakati wa kikao cha majadiliano ya ushirikiano baina Serikali hizo mbili kilicholenga mikakati ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Akiwasilisha salamu za Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bi. Mary Maganga, Dkt. Komba amesema Serikali ya Norway imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania katika sekta mbalimbali na kuongeza kuwa kwa sasa masuala ya mazingira yanazidi kupewa kipaumbele katika ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Dkt. Komba ameeleza Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Norway katika masuala ya usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali zinazopatikana baharini bila kuathiri hifadhi ya mazingira na kuanisha hatua mbalimbali zilizofikiwa katika juhudi za uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Akifafanua zaidi Dkt. Komba ameitaja moja ya miradi inayotekelezwa na Serikali ya Norway kupitia Shirika la Maendeleo la Norway NORAD ni pamoja na Mradi wa kujengea uwezo Taasisi zinazojishughulisha na masuala ya mazingira ili kupunguza hewa ukaa inayosababishwa na ukataji miti na uhalibifu wa Misitu (REDD+ READY) unaotekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Dkt. Komba amebainisha moja ya manufaa ya utekelezaji wa Mradi wa (REDD+ READY) ni pamoja uimarishwaji wa mifumo ya usimamizi endelevu ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo ambapo kumewezesha kupungua kwa uhalibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti na uchomaji wa misitu.
“Mabadiliko ya tabianchi yapo na upo uwezekano wa kukabiliana nayo, kwa kuwa ardhi bado ipo tunaweza kurejesha uoto wa asili ili vizazi vijavyo viweze kunufaika.
Serikali imeendelea kuchukua hatua muhimu za uhifadhi wa mazingira kwa kuendelea kushirikiana na wadau na wafadhili mbalimbali ikiwemo NORAD” amesema Dkt. Komba.
Kwa upande wake Mwakilishi wa masuala ya mabadiliko ya Tabianchi kutoka Ubalozi wa Norway, Bw. Odd Arnesen ameipongeza Tanzania kwa kuchukua hatua na jitihada mbalimbali za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikihatarisha usalama wa chakula.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na viongozi, maofisa waandamizi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.