Dkt. Mpango akaribisha wawekezaji EU
MAKAMU wa Rais Dkt Philip Mpango, amewakaribisha wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya (EU), kuwekeza nchini na kusema Tanzania imedhamiria kuvutia uwekezaji kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Akizungumza leo, wakati akifungua Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Dkt Mpango aliwakaribisha kuwekeza katika sekta za kilimo, usafirishaji, nishati na Tehama.
Maeneo mengine aliyoyataja ya kuwekeza ni utalii na katika viwanda vya kuongeza thamani, huku akisema serikali inahitaji kufungua zaidi sekta hizo, ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tanzania ipo katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka mingine 25, ambayo inalenga kubadilisha uchumi wa Taifa kutoka katika hali ya uchumi wa kati wa chini hadi kufikia uchumi wa kati wa juu ambapo kwa kiasi kikubwa unahitaji biashara na uwekezaji,” alisema Makamu wa Rais.
Aliwahakikishia wawekezaji mazingira mazuri na salama na kusema serikali inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.
Akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwekeza Tanzania, Dkt Mpango alisema uwekezaji utanufaika na soko kubwa la ndani la watu milioni 61.7, soko la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki la watu wasiopungua milioni 177, Soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) la zaidi ya watu milioni 300 pamoja na Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) linalojumuisha nchi 55 za Afrika zenye soko lisilopungua watu bilioni 1.4.