Serikali imewataka Wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini kuzingatia Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira zilizoainishwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi Mazingira(NEMC) wakati wa uanzishaji, uendelezaji wa viwanda nchini.
Agizo hilo limetolewa Februari 22, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ambayo imelenga katika kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya mazingira. Mhe Khamis amefanya ziara hiyo katika viwanda vya Multi Cable Ltd na Nyakato Steel Mills Ltd vilivyopo Wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza.
Akizungumza Naibu Waziri ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuinua uchumi wa viwanda ili kuweza kukuza Pato la Taifa, kukuza wigo wa ajira kwa vijana na kutengeneza uhusiano mzuri baina ya Serikali na wawekezaji, hivyo yapo masuala muhimu ya kimazingira yanayopaswa kupewa kipaumbele na wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo nchini.
Mhe. Khamis ameyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na viwanda kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya shughuli za mazingira katika jamii inayozunguka mradi wa uwekezaji ambapo wamiliki hawana budi kusaidia vifaa muhimu vinavyosaidia usafi wa mazingira katika eneo husika.
Aidha, amesema jambo lingine muhimu ni pamoja kutenga bajeti maalum ya utunzaji na upandaji miti pamoja na Mpango Kabambe wa kubadiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili nchi na dunia kwa ujumla.
“Nimetembelea na kuona uzalishaji katika kiwanda cha Multicable kuna matumizi ya miti ya asili tuliyoipanda. Kwa tafsiri ya haraka hapa tumeharibu mazingira, nawakumbusha wamiliki kuwasiliana na Ofisi yetu ya NEMC ili kuweza kuingia katika teknolojia ya kisasa ya nishati mbadala,” amesema Naibu Waziri Khamis.
Naibu waziri huyo pia amewakumbusha wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini kuhakikisha wanadhibiti utiririshaji wa majitaka kutoka viwandani kwenda katika makazi ya wananchi sambamba na kuiagiza NEMC Kanda ya Ziwa kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuona utekelezaji wa maagizo hayo aliyotatoa kwa wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutembelea Wilaya hiyo kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya mazingira katika Wilaya hiyo ambayo imekuwa na idadi kubwa ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Kwa niaba ya Wilaya, nakushukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kutenga muda na kutembelea Viwanda vilivyopo Ilemela. Nitoe wito kwa ofisi yako kutenga muda zaidi wa kufanya kaguzi za kimazingira ikiwemo kelele na mitetemeko ya sauti katika maeneo ya burudani na starehe” amesema Mhe. Masala.
Kwa upande wake Meneja uzalishaji Kiwanda cha Multi Cable Ltd, Hamisi Maleta amesema kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2004 kinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za plastiki za majumbani pamoja na vifaa vya umeme, kimekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira kwa kupunguza mrundikano mkubwa wa taka katika maeneo ya mjini ambazo ni malighafi muhimu za kiwanda hicho.
Aidha Maleta amesema miongoni mwa changamoto inayokikabili kiwanda hicho kwa sasa ni upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme kwani umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta athari katika uzalishaji wa bidhaa kiwandani hapo.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Alfred Yonas amesema ofisi yake imepokea changamoto zote zilizopo katika kiwanda hicho ikiwemo upatikanaji wa maji na kuahidi kukifanyia kazi kwa wakati.
Niwaombe wamiliki wa kiwanda waendelee kuvuta subira kwani mwezi mwezi April tunakwenda kuzindua mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh.bilioni 4 na hii itasaidia kumaliza changamoto hii hapa kiwandani,” amesema Yonas.