Habari

Jafo asema nishati safi ya kupikia inajumuisha mbinu zote zinazomuwezesha mtu kuandaa chakula bila kuathiri misitu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema nishati safi ya kupikia inajumuisha mbinu zote zinazomuwezesha mtu kuandaa chakula bila kuathiri misitu.

Amesema hayo wakati akishiriki mjadala wa Nishati Safi ya Kupikia kwenye kipindi cha Mizani kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1 tarehe 08 Mei, 2024 jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali katika kuhimiza nishati safi unalenga si tu la kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa bali pia kuhamasisha ubunifu wa nishati mbadala.

Amesema lengo namba saba la nishati safi ya kupikia ni lengo endelevu la dunia na linajibu malengo mbalimbali yaani ugunduzi na tafiti kwa watu mbalimbali kugundua unafuu wa nishati.

Halikadhalika, Dkt. Jafo ameeleza kuwa ubunifu unaozungumziwa ni namna mtu anavyoweza kutumia nishati za aina mbalimbali zikiwemo majiko ya gesi, majiko ya umeme, majiko, majiko ya nishati jadidifu na mbinu nyingine zozote zitakazomfanya mtu apike chakula.

“Malengo ya Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi na kuangalia namna gani wanavyoweza kuja na ubunifu hasa katika kumpa unafuu mwananchi wa kawaida kwa mfano anaweza kuwa na elfu mbili halafu akajaziwa gesi,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi za Serikali zimewezesha kampuni nyingi kuwekekeza katika gesi na wananchi kufungiwa majumbani kwao, hivyo kuleta fursa katika nishati safi ya kupikia.

Pia, baadhi ya kampuni zimewezesha shule kadhaa kuwa na mifumo ya gesi ambapo wanatumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia wanafunzi hivyo kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha watu Zaidi ya mia moja kuacha kutumia kuni na mkaa

Back to top button