Balozi wa Tanzania nchini Misri akutana na Naibu Balozi wa Iraq
Katika juhudi za kuzidi kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Iraq, Mhe Balozi amekutana na Mwenyeji wake Kaimu Balozi wa Iraq Dr. Arwa Hashim Abdol-Mohsin katika Ubalozi wa Iraq nchini Misri.
Ziara hiyo iliyofanyika siku ya tarehe 18 Januari, 2024 inakuja baada ya Mhe. Balozi Mej Gen. Richard M. Makanzo kuona kuna umuhimu wa kufungua kurasa mpya za kuzidi kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Katika yaliyojiri kwenye kikao hicho ni pamoja na Mhe. Balozi wa Tanzania kumueleza kwa kina fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania katika sekta ya kilimo, uvuvi, madini, viwanda, utalii na usafiri wa anga.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa makubaliano hasa katika sekta ya mafuta ikizingatiwa kuwa Iraq ni mzalishaji mkubwa wa nishati hiyo.
Nae kwa upande wake Naibu Balozi wa Iraq alifurahishwa sana na maelezo ya Mhe. Balozi na kuonesha utayari wa kufanya nae kazi bega kwa bega katika kuhakikisha wanakuza na kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, pia kuwapa mwamko raia wa Iraq na kuwashajiisha ili waweze kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.