DKT. BITEKO APONGEZA JUHUDI ZA RAIS DKT. SAMIA KUSTAWISHA DEMOKRASIA NCHINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kustawisha ustawi wa kidemokrasia nchini, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuwaletea Maendeleo watanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 4 Januari, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini ulioshirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ili kujadili miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria za Vyama vya Siasa.Mkutano umeandalilwa na Baraza la Vyama vya Siasa.
Miswada iliyokuwa ikijadiliwa ni muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.
“ Rais wetu amekuwa ni mfano wa kuigwa, kitaifa na kimataifa kwa kuhakikisha kuwa demokrasia yetu inazidi kustawi na kuifanya Serikali kuendeshwa kwa misingi ya haki, utawala bora na kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea na bila kusahau kuzingatia maoni ya watu ambao ni muhimu katika kuboresha utendaji wetu.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amepongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuandaa mkutano huo ambao ni muhimu kwa maslahi ya Taifa na kueleza kuwa Baraza hilo kwa kwa mujibu sheria linajukumu pia la kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa na masuala mengine yanayohusu vyama vya siasa na demokrasia.
Amesema kuwa, mkutano huo umekuwa wenye tija kwani washiriki wameweza kutoa maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa wajumbe wa Mkutano huo kuitikia wito wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson wa kwenda bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari ili kutoa maoni kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi na mswada wa sheria ya vyama vya siasa.