Habari Tofauti

Mhe.Pindi Chana Aipongeza TAMISEMI Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati 

Na Fred Kibano

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pindi Chana ameipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuhamasisha Wadau wa mazingira ili kutunza mazingira nchini.

Mheshimiwa Pindi Chana ameyasema hayo mapema leo kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Nzuguni Jijini Dodoma alipotembelea banda la Ofisi ya Rais TAMISEMI kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa ambapo ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendeleza malengo ambayo yamejikita kuwahudumia wananchi.

Awali akitoa maelezo baada ya kumkaribisha mgeni rasmi Mheshimiwa Pindi Chana, Bwana Rogasian Lukoa Afisa Misitu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema jukumu kubwa la Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kusimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na kusimamia na kuendeleza shughuli za Serikali za Mitaa ambapo kwenye maonesho hayo ni pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma na kazi za Ofisi ya Rais TAMISEMI lakini pia kuhamasisha utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi hususani nishati mbadala ya kupikia.

Baada ya mgeni rasmi kutembelea mabanda ya maonesho kutakuwa na tukio maalum kwa siku ya leo ambalo ni Kongamano la Mtama lenye kauli mbiu ‘Mtama, Uhakika wa Chakula’

Mheshimiwa Pindi Chana ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mheshimiwa Jabir Shekimweri.

Maonesho Nanenane kwa Kanda ya Kati yanaendelea kwenye viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma ikiwa leo ni siku ya nne tangu kuanza na yalifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule.

Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu ni “Vijana na wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya hakula”

Back to top button