Habari Tofauti

DED AELEKEZWA KUMLIPA FUNDI ANAYEJENGA MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI MLIMA SHABAHA “B”

James Mwanamyoto

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bw. Dionis Myinga kumlipa fundi aliyepewa kandarasi ya kujenga miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa na jengo la utawala katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B” kupitia mradi wa BOOST ili akamilishe ujenzi wa miundombinu hiyo kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, akiwa Wilayani Hai wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B” mara baada ya kubaini kasi ndogo ya ujenzi iliyosababishwa na Halmashauri kutomlipa fundi madai ya fedha zake.

Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kulipa uzito suala la usimamizi na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya elimu, kwani Serikali imepeleka fedha nyingi ili ikamilike kwa wakati na hatimaye wanafunzi wanufaike kwa kupata elimu bora.

“Fedha hizi zimeletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwawezesha mafundi kukamilisha jukumu la ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa manufaa ya taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amewata watendaji Serikalini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa uzalendo kama ambavyo Mheshimiwa Rais anavyopambana kutafuta fedha ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Hai Mhe. Saasisha Mafuwe amesema kumekuwa na changamoto ya mafundi kutolipwa kwa wakati licha ya Serikali kuwasilisha fedha katika Halmashuri ya Hai hivyo ameutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kutekeleza maelekezo ya Mhe. Ndejembi ili wananchi wanufaike na miundombinu ya elimu inayojengwa.

Sanjari na hilo, Mhe. Mafuwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili kujenga miundombinu ya elimu na barabara.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa amesema kuw amepokea maelekezo ya Mhe. Ndejembi na kuongeza kuwa yeye pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama watahakikisha ujenzi wa miundombinu ya elimu unatekelezwa usiku na mchana ili Halmashauri ya Hai isiwe ni kikwazo cha jitihada za Serikali kuboresha elimu nchini.

Back to top button