RAIS DK.MWINYI ASEMA WATOAJI MSAADA WA SHERIA NI KIUNGO CHA HAKI NCHINI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema watoaji msaada wa kisheria ni kiungo muhimu cha upatikanaji wa haki nchini hasa kwa wananchi wasio na uwezo wa fedha kwa msaada wa sheria nchini.
Ameyasema hayo leo alipohutubia katika kilele cha Maadhimisho ya wiki msaada wa sheria mwaka 2023 na utoaji wa Tuzo za Mwaka kitaifa kwa watoa msaada wa kisheria Zanzibar yaliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakil Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha , Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itahakikisha marekebisho ya sera na sheria ya msaada wa sheria yanafanyika haraka na kwa ufanisi ili kukidhi matakwa yanayotakiwa kwa utoaji wa msaada wa sheria nchini.
Vilevile, amezipongeza taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kwa juhudi wanazochukua kuwafikia wananchi na kuwafahamisha juu ya upatikanaji wa huduma za sheria nchini.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itashughulikia kwa haraka masuala yanayowahusu watoaji wa huduma wa msaada wa sheria nchini ikiwemo vitendea kazi vya ofisi na changamoto ya usafiri .