Habari

WAZIRI MKUU: AKINABABA MUWASAIDIE WAKE ZENU KULEA WATOTO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka jamii ishirikiane na akinamama katika malezi ili kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania.

Ametoa wito huo jana usiku (Jumapili, Mei 14, 2023) wakati akizungumza na washiriki  wa hafla ya Mtoko wa Mama kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani. Hafla hiyo iliandaliwa na taasisi ya Binti Lindi Initiative.

“Akinababa washirikiane na akinamama katika malezi ya watoto kwani kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tumelelewa na akinamama zaidi, lakini akinababa tunapaswa vilevile kujipa muda na kufuatilia mwenendo wa tabia ya mtoto kuanzia asubuhi mpaka usiku,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa jamii kuheshimu na kuthamini mchango wa mama katika malezi. “Kama wahenga walivyosema, kuzaa siyo kazi ila kazi ni kulea mwana, tushirikiane na akinamama wote katika malezi ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania,” amesema.

“Ninatambua kuwa mama zetu katika karne hii mnafanya shughuli nyingi za kiuchumi kwa ajili ya ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla. Niwasihi sana muendelee kuwa vinara katika suala la malezi ya watoto,” amesisitiza.

Amewataka wazazi na walezi wajitambue kuwa wao ni taasisi muhimu tena ya kwanza katika malezi ya mtoto. “Timizeni wajibu wenu, shirikianeni na taasisi za kiserikali ili kukuza na kuimarisha maadili kwa watoto wenu pamoja na kutenga muda wa kuwafuatilia ili kujua changamoto zao na kuwelea ipasavyo.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Mwanaidi Ali Khamisi alisema Siku ya Mama Duniani huadhimishwa kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei kila mwaka.

Alisema kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto na wizara yake iliamua kuunda madawati ya watoto kwenye shule zote za msingi na sekondari ili wapate mahali pa kujieleza pindi wakiona dalili ama wakifanyiwa ukatili.

Back to top button