Uchumi

TANZANIA: MIRADI 630 YA UWEKEZAJI YENYE THAMANI YA SH. BIL. 3.68 YASAJIWA NA TIC

0:00

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 miradi mipya ya uwekezaji 630 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.68 inayotekelezwa na makampuni ya India imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Amesema hatua hiyo inatokana na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka nchini India waje wawekeze Tanzania.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi 19 Januari 2023) wakati alipokutana na ujumbe wa Bunge la India (Lock Sabha) ulioongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mheshimiwa OM Birla. Waziri Mkuu kutana na viongozi hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ambaye yupo nje ya nchi kikazi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Nchi ya India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano Mkubwa wa kiuchumi na biashara huku India ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na ushirikiano wa biashara unaofikia Dola za Marekani bilioni 4.58 kwa mwaka 2021 – 2022.

Waziri Mkuu amemuhakikishia Spika huyo kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na India. “Rais anamatumaini makubwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi ya Tanzania na India na kwamba ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa kati ya nchi zetu.”

Amesema Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali zikiwemo za uchumi, nishati, maji, elimu, afya, biashara na teknolojia na hivyo kuleta manufaa makubwa.“Mheshimiwa Rais amefurahia ujio wako Nchini Tanzania, ni matarajio yake kuwa ujio huu utakuwa na manafuu makubwa baina ya Nchi zetu.”

“Mwezi juni 2022 tumeshuhudia makampuni sita kutoka nchini India yakitia saini mikataba ya miradi ya maji kwa miji 28 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 500 ambayo ikikamilika itawawezesha watanzania zaidi ya milioni sita kupata maji ya uhakika.”

 

Back to top button