Habari

RAIS DKT.MWINYI AKUTANA NA RAIS WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA

Ahmed Hassan

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Jumamosi Februari 25, 2023 ameupokea ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, ukiongozwa na Rais wake Dkt.Akinwumi Adesina Ikulu, Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuunga mkono miradi mbalimbali ya Maendeleo Zanzibar ikiwemo ya kijamii katika sekta ya Afya , barabara, maji na sekta ya usafiri.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo wa Benki ya Maendeleo juu ya hatua zinazoendelea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia sekta zilizo chini ya uchumi wa buluu ambapo kwa upande wa utalii amewaeleza unachangia asilimia 30 ya pato la nchi.

Naye, Rais huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt . Adesina alimuelezea mwenyeji wake Rais Dkt. Mwinyi miradi ambayo Benki hiyo inasaidia zaidi ujenzi wa barabara na sekta nzima ya usafiri.

Alisema kwa sasa Benki yake inasaidia ujenzi unaoendelea wa barabara ya Bububu-Mahonda-Mkototoni, ujenzi wa barabara Tunguu-Makunduchi na ya Mkoani- ChakeChake.

Vilevile benki hiyo imejikita kusaidia ujenzi wa Uwanja wa ndege mpya wa Pemba na miradi kadha ikiwemo ya maji na ujenzi wa masoko pia tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika imetenga dola za Kimarekani milioni 15 kuunga mkono sekta zilizochini ya Uchumi wa Buluu.

Back to top button