Rais Samia asaini miswada mitatu
SPIKA wa Bunge, Dkt Tulia Ackson amelieleza Bunge kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesaini miswada mitatu iliyopitishwa katika Bunge la tisa iwe sheria.
Dkt Ackson alisema bungeni Dodoma jana kuwa, miswada iliyopitishwa na bunge hilo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa mwaka 2022.
Mwingine ni Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022 na Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2022.
Dkt Tulia alisema kwa kuwa Rais Samia amesaini miswada hiyo, sasa itafahamika kwa jina la Sheria ya Uwekezaji Tanzania Namba 10 ya Mwaka 2022, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa za Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022 na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 12 ya Mwaka 2022.
Wakati huo huo, alimuapisha Abdul Yussuf Maalim kuwa Mbunge wa Jimbo la Aman visiwani Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Maalim anachukua nafasi iliyoachwa wazi baada ya kufariki dunia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Hassan Mussa.