Leo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji wa Ngulyati – Nyamswa Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu pamoja na kukabidhi mitambo ya kuchimba visima virefu vijijini iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 utatoa huduma kwa wananchi 10,106 wa vijiji vya Ngulyati, Nyamswa na Nyasosi.
Mradi huo umeanza kutoa huduma una uwezo wa kuzalisha maji lita 15,800 kwa saa sawa na lita 284,000 kwa siku.
Akitoa Taarifa ya Mradi huo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala amesema mahitaji ya ya Maji katika vijiji hivyo vitatu ni Lita 271, 900 hivyo uzalishaji wa maji katika mradi huo unajitosheleza.
Akizungumzia mradi huo Waziri Mkuu, amesema mradi huo ni muendelezo wa kampeni ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.