MAMA MARIAM MWINYI ATANGAZA KAMPENI YA “AFYA BORA, MAISHA BORA” TAREHE 30 SEPTEMBA MKOA WA MJINI MAGHARIBI
Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Mhe.Mama Mariam Mwinyi amesema ZMBF imeandaa kampeni ya “Afya Bora,Maisha Bora” inayolenga kuweka kambi maalumu ya kupima afya na matatibu bure kwa siku tatu kuunga mkono juhudi zinazofanywa kwa vitendo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kampeni hiyo itazinduliwa kupitia Mariam Mwinyi Walkathon itakayofanyika viwanja vya Dole, Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi kuanzia tarehe 30 Septemba 2023 hadi tarehe 02 Oktoba, 2023.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 11 Septemba 2023 alipozungumza na uongozi wa Hospitali ya Kitengule kutoka Dar es Salaam waliofika ofisi za ZMBF Ikulu Migombani.
Aidha, Mama Mariam Mwinyi amewashukuru na kuwapongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kufanikisha kambi maalumu ya matibabu na upasuaji iliyofanyika Hospitali ya Kitogani Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Vilevile, Hospitali ya Kitengule imemkabidhi Mama Mariam Mwinyi msaada wa madawa mbalimbali ikiwemo ya magonjwa ya presha, sukari na vifaa tiba kwa ajili ya upasuaji.