Habari

MCHENGERWA ATOA MWEZI MMOJA KWA DED MULEBA KUKAMILISHA UJENZI WA HOSPITALI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya  Muleba Dk.Peter Nyanja kukamilisha majengo ya hospitali ya Wilaya.

Pia ametoa siku nne kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Elias Kayandabila (ambaye sasa ni DED Tabora Manispaa) na mhandisi Zefania Chacha kutoa maelezo ya kwanini fedha zilizotengwa Sh. milioni 500 zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo.

Ofisi ya Rais-TAMISEMI iilitoa Sh milioni 500 kwa kila Halmashauri isiyo na hospitali ya Wilaya kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje na maabara.

Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo hayo  baada ya kutemebelea hospitali hiyo na kuutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kutumia mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa magonjwa ya wagonjwa wa nje na maabara ili wananchi aanze kupata huduma wakati majengo mengine ya namalizia.

Alisema kwa kutumia mapato ya ndani Mkurugenzi ahakikishe anamaliza ujenzi wa majengo hayo na kuwa ifikapo Januari,2024 atakuja kukagua ili wananchi wapate waanze kupata huduma.

“Mnakwenda kufanya mapitio ya Bajeti zenu, hakikisheni mnatenga fedha kwa ajili ya majengo haya ili nikija Januari iwe limekamilika kinyume chake nitakusimamisha na kupeleka jina lako kwa Mheshimiwa Rais ili akutengue.

” Kwa walioshindwa kumalizia majengo, Mhe. Mchengerwa alisema inashangaza kuwa serikali inatoka fedha kwa ajili ya miradi lakini baadhi ya Watumishi wanazitumia ndiyo sivyo na kusisitiza kuwa hata kama Mkurugenzi amehama kituo cha kazi lazima atoe maelezo na yafike Ofisini kwake Jumatano ijayo.

“Haiwezekani Rais Samia awaletee wananchi wake fedha za kuwajengea hospitali lakini wengine wanazitumia vibaya hiyo Haiwezekani na wala sitakubali hali kama hiyo.”

Alisema fedha ambazo Waziri Mkuu aliahidi ya Shilingi bilioni 1 Serikali itazileta Januari mwakani na kuwa fedha hizo itatumika kujenga majengo mengine ya hospitali.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa alisema changamoto iliyokuwepo ni usimamizi dhaifu wa miradi na kuwa ameelekeza kutumia mapato ya ndani kukamilisha majengo hayo.

” Halmashauri zingine ambazo ziko mbali zaidi ya hii na maeneo yao yalikuwa mabaya wamekamilisha na majengo yao ni mazuri, shida iko hapa Muleba na Bukoba.”

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk. Abel Mwendawile alisema tayari walishaielekeza TAKUKURU kupitia gharama za ujenzi wa hospitali hiyo.

Naye Dk.Nyanja alisema ili kukamilisha majengo hayo kiasi cha Sh milioni 191.9 zinahitajika na kuahidi kuzitafuta wakati wa kufanya mapitio ya Bajeti ya mwaka 2023/24.

Back to top button