Waziri Mkuu Atoa Agizo kwa Watendaji wa Serikali
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali wasiwe kikwazo, waendelee kutoa ushirikiano kwa viongozi wa dini na wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji na kushirikiana na sekta binafsi pamoja na madhehebu yote ya dini katika kutekeleza majukumu mbalimbali.
“Katika hili nasisitiza watendaji wote wa Serikali kuendelea kuziunga mkono taasisi binafsi zinazotoa huduma kwa wananchi ili ziweze kutimiza malengo yake.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 20, 2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya Chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini Arusha.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Askofu Mkuu wa Makanisa ya International Evangelism na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Eliud Issangya kwa kuongoza vema chuo hicho ambacho kimetimiza miaka 40.
“Nimefurahi sana kusikia idadi ya wahitimu wa chuo hiki imefikia zaidi ya 10,000 ama kwa hakika mmeweza kuweka hazina kubwa ya watendaji katika shamba la Mungu”.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho ikiwemo ya barabara, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TARURA mkoani Arusha kuhakikisha barabara hiyo ya kutoka Kikatiti hadi Sakila inakarabatiwa.
Naye, Dkt. Issangya amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha maridhiano na kuwatia moyo viongozi wa dini, hivyo kuwawezesha kutekeleaza majukumu yao kwa urahisi.
Amesema uimara wa Serikali umewawezesha viongozi wa dini zote nchini kupendana, kufanya kazi kwa kushirikiana, kuaminiana na kuheshimiana.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la International Evangelism la nchini Congo, Askofu Byamungu Magala ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu.
“Tanzania ni Taifa ambalo limejaa amani na utulivu na ni Taifa ambalo halina ubaguzi wa dini wala kabila, Taifa zuri linalopokea wageni bila ya shida yoyote. Nawapongeza viongozi wa Taifa hili,” amesema Askofu Magala.