Habari Tofauti

RAIS DK.MWINYI APANDISHA PENSHENI KWA WASTAAFU NA WAZEE ZANZIBAR

Ahmed Hassan

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itapandisha pensheni kwa  wastaafu  kwa asilimia mia moja akitolea mfano wa mstaafu wa kima cha chini anayepokea   shilingi  elfu 90,000/= atapanda mpaka shilingi 180,000/=. Ametekeleza ombi la wastaafu hao  walilolitoa mwaka jana .

Ameyasema hayo leo tarehe 01 Mei 2023  katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Viwanja vya Skuli ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais Dk. Mwinyi amesema  Serikali itapandisha pensheni jamii kwa asilimia mia moja na hamsini kwa Wazee kuanzia miaka 70 ambapo kwa sasa wanaopata  elfu ishirini watapanda hadi  shilingi elfu hamsini.

Utekelezaji wa mabadiliko hayo utaanza Mwezi Julai mwaka mpya wa bajeti utakapoanza.

Serikali inashukuru kwa namna Wafanyakazi walivyopokea kwa furaha mabadiliko ya mishahara yaliyofanyika.

Vilevile Dk.Mwinyi amesema mipango na mikakati ya Serikali ni kuimarisha uwajibikaji kwa kuzingatia namna ya kuboresha mazingira ya kufanyia kazi yakiwemo mishahara bora na stahiki nyengine za watumishi.

Dk  Mwinyi amesema serikali ipo hatua za mwisho za kuanzisha mfumo wa Bima ya afya kwa wafanyakazi wote umma Zanzibar.

Amesema Serikali imepokea ombi  la Wafanyakazi kupatiwa fedha za nauli kuwawezesha kwenda kazini  na kurudi nyumbani nje ya mishahara yao.

Back to top button