
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge watambue mchango wa Asasi za kiraia katika kazi zao kwa kuwa zina changia maendeleo Taifa.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 28, 2023) alipofungua mafunzo ya kamati ya uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, kwenye ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu, Kusini Unguja Zanzibar
“Sote tunafahamu mchango wa asasi za kiraia nazo pia lazima tuzifahamu, tunazo asasi za kiraia ambazo tumeweka mikataba nayo, ni muhimu kulizingatia, uwezo wa Serikali pekee hautoshi, Bunge mtapata fursa ya kukutana nazo kwenye kamati zenu, lazima mtambue mchango wake na uwe na maslahi kwa Taifa”
Amesema kuwa ni muhimu kamati hizo kuhakikisha asasi hizo zinatekeleza majukumu ya kimsingi ambayo wamekubaliana na Serikali kwa maslahi ya jamii yetu na si kubeba ajenda ambazo hazina maslahi kwa jamii yetu.
“Ni muhimu sana viongozi wenzangu mkazingatia yale mambo ambayo yanavunja maadili, miiko, mila na utamaduni wetu, sisi wabunge ukiwa kwenye kamati yako ukiona moja ya asasi inaenda kinyume na yale tuliyokubaliana msiache kuyaleta mezani, malengo ya kamati hii ya uongozi ni kuishauri Serikali kuendesha nchi katika kukuza maslahi yetu kimaendeleo na maadili tuliyonayo”.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Wajumbe kukaa pamoja na kukumbushana masuala mbalimbali, kujadili mafanikio na changamoto pamoja na kuweka mikakati ya kiuendeshaji na utendaji wa Kamati za Bunge na Bunge kwa ujumla.
“Ni matumaini yangu kwamba wajumbe na washiriki wa mkutano huu watatumia vizuri fursa hii ya kuwa hapa pamoja kujifunza, kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Bunge”.