WAZIRI MKUU AALIKA WAWEKEZAJI VIWANDA VYA MBOLEA
*Ashiriki ufunguzi wa Jukwaa la Uchumi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaalika wawekezaji waliobobea kwenye sekta ya mbolea ili waje kufungua viwanda vya mbolea nchini.
Ametoa mwaliko huo leo (Alhamisi, Julai 27, 2023) wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu Uimarishaji wa Soko la Mbolea kama njia ya kuondoa njaa barani Afrika uliofanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.
Amesema uamuzi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuongeza bajeti ya kilimo una nia ya kuifanya Tanzania iwe eneo la uzalishaji la kulisha Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika. “Bado tuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa sababu ikikosekana inaathiri uzalishaji wa chakula.”
“Mbolea kwa sasa ndiyo msingi wa uzalishaji chakula. Uzalishaji wetu unatumia zaidi ya asilimia 80 na kwa maana hiyo tunalazimika kutumia fedha nyingi ili kuagiza mbolea kutoka nje na msisitizo wa sasa ni kuzalisha mbolea yetu.”
“Tunatumia fursa hii kutafuta marafiki ambao wako tayari kuja kuwekeza kwenye mbolea. Mahitaji yetu ni zaidi ya tani 800,000 wakati uzalishaji wetu ni tani 200,000. Tumeshapata kiwanda ambacho kinazalisha mbolea na sasa wameshafikisha tani 400,000 na wanalenga kufikia tani 800,000 lakini hatuwezi kuetegemea kiwanda kimoja peke yake,” amesema.
Amesema Tanzania ina rasilmali ya gesi ambayo inaweza kutumika kutengeneza mbolea ukiacha zile za kawaida za wanyama. “Tukifanikiwa kuongeza uzalishaji wa mbolea, tutakuwa na nafasi ya kuzalisha chakula zaidi. Jukwaa hili ni nafasi pekee ya kualika wawekezaji waliobobea kwenye maeneo kama haya,” amesisitiza.
Mapema, Waziri Mkuu alishiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu lililofunguliwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.