Habari Tofauti

UNEP KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UHIFADHI WA MAZINGIRA

Naibu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Bi.Elizabeth Mrema ameeleza kuwa  Shirika hilo litaendelea kuimaisha mashirikiano na Tanzania katika jitihada za kuhifadhi mazingira  ikiwemo utekelezaji wa miradi.

Bi Elizabeth ameyasema hayo katika kikao cha pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi Mary Maganga, kikao kilichofanyika leo tarehe 10 Agosti,2023 Jijini Nairobi, Nchini Kenya.

Katika kikao hicho,vipaumbele vya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania viliwasilishwa na kujadliwa. Maeneo yaliyojadiliwa ni Hali ya Mazingira nchini pamoja na Jitihada za kukabiliana na changamoto za mazingira.

UNEP iliombwa kuwezesha  utekelezaji  wa miradi mbalimbali iliyoandaliwa na kutajwa kwenye Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira 2022-2032; Kujenga uwezo wa Kitaasisi  na wataalamu  katika usimamizi wa mbinu za masoko na zisizo za masoko za upunguzaji wa gesi joto ikiwemo biashara  ya kaboni; Kufanya tathmini ya fursa za uwekezaji katika biashara ya Kaboni, udhibiti wa taka pamoja na kuimaisha ushiriki wa sekta binafsi katika Hifadhi ya Mazingira.

Akijibu maombi hayo  Naibu Mtendaji Mkuu wa UNEP Bi.Mrema ameihakikishia Serikali ya Tanzania kwa UNEP itaendelea Kujenga uwezo wa wataalamu na Taasisi za elimu ya juu  nchini katika kuandaa miradi ambayo wafadhili wataweza kuifadhili pamoja na  kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya kazi za kujitolea katika Shirika hilo.

Aidha katika kikao hicho , fursa mbalimbali za upatikanaji wa raslimali fedha kupitia washirika wa maendeleo ziliwasilishwa. MWISHO.

زر الذهاب إلى الأعلى