Siasa

WENYEVITI WATATU WA BUNGE WACHAGULIWA

Ahmed Hassan

Bunge limewachagua Wenyeviti watatu wa Bunge ambao watasaidia katika kuongoza vikao vya Bunge kwa maelekezo ya Spika wa Bunge au Naibu Spika kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.

Waliothibitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Wenyeviti wa Bunge mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi kupendekeza majina yao ni pamoja na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum na Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Daniel Baran Sillo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufundi Kusini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo

Akizunguza Bungeni, Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Akcson amesema utaratibu wa kuwapata Wenyeviti wa Bunge umewekwa katika Kanuni ya 13 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Aidha alisema kuwa katika chaguzi zinazofanyika Bungeni iwapo idadi ya wagombea inalingana na nafasi zilizopo na vigezo vinavyohitajika vimetimizwa basi wagombea hao wanapita bila kupigwa.

Aliongeza kuwa utaratibu kama huo ulitumika kwenye uchaguzi wa Wenyeviti wa Bunge katika Bunge la Kumi, Bunge la Kumi na Moja na katika Bunge hili la Kumi na Mbili ambapo; Kamati ya Uongozi ilipendekeza majina matatu na baadaye majina hayo yalithibitishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Hivyo kwa muktadha huo, Mheshimiwa Spika aliwahoji Waheshimiwa Wabunge ili kuthibitisha Waheshimiwa hao waweze kuwa Wenyeviti wa Bunge.

Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Najma Giga aliwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Kamati ya Uongozi kwa kumuamini kwa mara nyingine tena.

“Wahesimiwa Wabunge nawashukuru kwa kuniamini tena nawaombeni ushirikiano na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu naamini atanisaidia katika kutekeleza majukumu yangu,” alisema.

Kwa upande wake Mheshimiwa David Kihenzile alimshukuru Mheshimiwa Spika na Wabunge wote kwa kumuamini na kumthibitisha tena kuwa Mwenyekiti wa Bunge.

“Nakishukuru pia Chama changu kwa imani waliyonionesha nawaahidi ushirikiano, unyenyekevu na utiifu mkubwa katika utumishi wangu,” alisema.

Naye Mheshimiwa Daniel Sillo aliwashukuru Waheshimiwa Wabunge na kuipongeza Kamati ya Uongozi kwa kumuamini na kumpitisha.

“Nakishukuru pia chama changu, nawaahidi ushirikiano na pia nawaombeni ushirikiano ili tuweze kutekeleza jukumu hili la kumsaidia Spika katika uendeshaji wa Bunge,” alisema.

Kwa upande mwingine Spika wa Bunge aliwapongeza Wenyeviti hao kwa kuchaguliwa na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuwapatia ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao vyema.

زر الذهاب إلى الأعلى