WASANII WALINDWE ILI WAONE MATOKEO YA KAZI ZAO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha inawasimamia, kuwalinda na kutoa elimu kwa wasanii wote nchini kuhusu umuhimu wa kujisajili na kuwa na hati miliki ya kazi zao ili waweze kunufaika na mapato yanayotokana na kazi hizo.
Amesema ni vyema Wizara ikaweka utaratibu rafiki na msisitizo katika masuala muhimu yatakayo wawezesha wasanii kunufaika na fursa zilizowekwa na Serikali ikiwemo mikopo nafuu kwa ajili ya kununua vifaa sambamba na uzalishaji wa kazi za sanaa.
“Wasanii wote tumieni fursa ya uwepo wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii ni Wizara kwa ajili yenu, changamkieni kila fursa zinazotolewa kupitia Wizara yenu. Itumieni vema kwani iko kwa ajili ya ustawi na maendeleo yenu.”
Ameyasema hayo jana (Jumapili Machi 31, 2024) alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha la nyimbo za Injili la Mtoko wa Pasaka lililofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki, Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali, imeendelea kuimarisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa lengo la kuwawezesha wasanii kuendeleza kazi zao kwa kuwapa mikopo sambamba na elimu ya ujasiriamali ambapo mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.39 imetolewa kwa miradi 113 ya Utamaduni na Sanaa na kuwafikia wasanii 230,685.
“Serikali imetoa mikopo kwa wasanii mbalimbali kununua vifaa vya kisasa vya Studio ili kupunguza adha kwa wasanii kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya uzalishaji wa kazi zao.
Aidha, ametoa wito kwa waumini wa madhehebu yote ya dini na Watanzania kwa ujumla, kutumia msimu huu wa sikukuu kuongeza upendo, kudumisha amani na kuhimiza mienendo mizuri kimaadili kwa kuzingatia mila na utamaduni wa kitanzania sambamba na kuyakana matendo maovu ikiwemo ya mauaji, wizi, visasi, wivu, ubakaji, unyanyasaji na ubadhilifu.