WAZIRI JAFO: WATANZANIA TUJIVUNIE MUUNGANO WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Watanzania hawana budi kujivunia Muungano uliopo kufuatia mafanikio lukuki yanayoendelea kupatikana kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaendelea kuwanufaisha wananchi.
Waziri Jafo ameyasema hayo Jumanne (Julai 11, 2023) Mjini Zanzibar wakati wa ziara yake ya kukagua miradi iliyojengwa kwa fedha za UVIKO 19 katika Halmashauri za Wilaya ya Unguja, Zanzibar huku akieleza kuridhishwa na ubora wa miradi hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wameendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuhakikisha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zinawafikia kwa wakati katika maeneo yote ya nchi ili kuharakisha kasi ya maendeleo kwa wananchi.
“Katika kipindi cha miaka miwili sote ni mashahidi tumeshuhudia kiasi kikubwa cha fedha takribani Bilioni 600 zimeletwa hapa Zanzibar kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo takribani Shilingi Bilioni 230 ambazo ni fedha za UVIKO 19 ambapo fedha hizo zimetimika kutekeleza miradi ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji” amesema Dkt. Jafo.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya miradi hiyo inalindwa ili iweze kuleta manufaa ya muda mrefu zaidi kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Awali akikagua mradi wa maji uliopo katika Kijiji cha Bambi Jimbo la Uzini, Zanzibar Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini, Mhe. Khamis Hamza Khamis ( Chilo) amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za UVIKO 19 ambazo zimesaidia kuleta mapinduzi makubwa ya miundombinu ya miradi ya maendeleo jimboni humo na Zanzibar kwa ujumla.
“Tunawashukuru Viongozi wetu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kwa maono yao makubwa ya kuhakikisha kuwa fedha za UVIKO 19 zinatumika katika miradi ya maendeleo. Mradi huu wa maji utaweza kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Uzini na maeneo ya jirani” amesema Mhe. Khamis.
Aidha akikagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya Mjini Magharibi, Zanzibar Waziri Jafo amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Uongozi wa mkoa na Wilaya ya Mjini Magaharibi katika kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo ambayo ni moja ya miradi ya kihistoria inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi.
“Hospitali hii ikikamilika itasaidia kusogeza huduma ya afya karibu na maeneo ya wananchi, hata hospitali ya Mnazi mmoja sasa itapunguziwa mzigo mkubwa wa wagonjwa ambao sasa watakuja kuhudimwa hapa.Nawapongeza viongozi hadi kufikia hatua hii ya mradi wa ujenzi” amesema Dkt. Jafo.
Katika hatua nyingine Dkt. Jafo pia ametembelea shule ya msingi Salim Turky iliyopo Jimbo la Mpendae, Zanzibar ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na walimu, watendaji na wanafunzi wa shule hiyo pamoja na kukagua maeneo mbalimbali ya shule ikiwemo maktaba, maabara na darasa la masomo ya TEHAMA.
Akiwa shuleni hapo Waziri Jafo ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa juhudi kubwa wanazoendelea kufanya katika kusimamia maendeleo ya taaluma shuleni na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa makubwa kwani serikali zote mbili zimedhamiria kwa dhati kuboresha miundombinu ya shule zote za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu nchini.
Waziri Jafo yupo katika ziara ya kikazi Zanzibar kwa ajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na Wabunge, Viongozi na Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo usimamizi wa fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo.