TOENI MOTISHA KWA WATOA HUDUMA ZA AFYA
Viongozi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini wameelekezwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wanaofanya vizuri ili kuwapa ari ya kufanya kazi kwa bidii ya kutoa huduma bora kwa jamii.
Maelekezo hayo yametolewa na Dkt.Ntuli Kapologwe Mkurugenzi wa Idara ya afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala Za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya tathmini na ukaguzi katika Mkoa wa Mwanza kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Mwanza.
“Viongozi wenzangu Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni mnaweka utaratibu wa kutoa motisha kwa watoa huduma za afya katika maeneo yenu lengo likiwa ni kuzidi kuwatia ari na Motisha ya kuwahudumia Wananchi.” amesisitiza Dkt.Ntuli.
Amefafanua kuwa Zawadi sio fedha ,pekee bali wanaweza kuweka utaratibu wa kutoa vyeti au kuwaandikia barua za pongezi na kutambua michango yao kwenye sekta kwa kuwa itawapa nguvu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, amewataka viongozi hao kutekeleza maelekezo hayo na kutoa mrejesho.