TAMISEMI YASISITIZA UFAULU MZURI SHULENI
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Vicent Kayombo amekagua miradi ya elimu inayotekelezwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kusisitiza ufundishaji wenye matokeo mazuri ya ufaulu.
Ziara hiyo ameifanya Julai 27, 2023 katika Shule ya Sekondari Kigoma, Shule ya Msingi Katubuka na Kabingo za Manispaa hiyo zinazoendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mkurugenzi huyo ameonesha kuridhishwa na namna miradi inavyotekelezwa na kuhimiza walimu kufundisha kwa bidii ili shule hizo ziwe na matokeo mazuri ya ufaulu.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwantum Mgonja amempongeza Mkurugenzi wa Elimu -TAMISEMI kwa namna ambavyo ametembelea shule hizo na kutoa ushauri wa kitaaluma huku akiahidi kuendelea kusimamia ili kuwa na ufaulu mzuri.
Katika Shule ya Sekondari Kigoma kuna ujenzi wa mabweni mawili, madarasa nane na matundu nane ya vyoo kwa gharama ya sh.milioni 419 fedha kutoka Serikali kuu.
Aidha, Shule ya Msingi Katubuka kuna ujenzi wa madarasa manne, moja ni kwaajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu na matundu matatu ya vyoo kwa gharama ya sh.milioni 136.6 huku shule ya Kabingo kukiwa na ujenzi wa madarasa manne na matundu manne ya vyoo kwa gharama ya sh.milioni 112.8 fedha za mradi wa BOOST.